Kenya imeripoti wagonjwa wapya 389 huku idadi yao ikifikia 7,577

Waziri wa Afya Kenya Mutahi Kagwe
Idadi ya wagonjwa wa virusi vya coroa nchini Kenya imeongezeka na kufikia 7,577 baada ya wagonjwa 389 wapya kuthibitishwa.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema siku ya Jumamosi kwamba kati ya wagonjwa hao watatu ndio sio raia wa Kenya.

Miaka ya wagonjwa waliothibitishwa ni kati ya mwaka mmoja hadi miaka 93.

Bwana Kagwe alisema katika taarifa yake kwamba kati ya wagonjwa hao wapya , 243 wanatoka Nairobi, 36 kutoka Kajiado, 27 kutoka Kiambu, 23 kutoka Mombasa, 17 kutoka Busia na 10 kutoka Machakos.

Kaunti nyengine mbazo zilirekodi wagonjwa wapya katika kipindi cha saa 24 ni Migori 4, Kitui 6, Makueni 3, Uasin Gishu 3, Nakuru 3, Kilifi 2, Garissa 1, na Narok 1.


Waziri huyo alitangaza kwamba watu 88 zaidi wamepona kutoka hospitali na kufanya idadi ya waliopona hadi kufikia sasa kuwa 2,236.

Wagonjwa wengine 5 hatahivyo walifariki na kufanya idadi ya waliofariki kufikia 159.

''Kupitia takwimu hizi , ni ishara kwamba tumepoteza maisha mengi, hatuwezi kukubali kupoteza maisha zaidi. Hivyobasi sisi kama taifa ni sharti kuheshimu masharti ya kukabiliana na ugonjwa huu la sivyo ugonjwa huu unaweza kuathiri vifaa vyetu vya afya'', alisema Kagwe.

Madai hayo ya Kagwe yanajiri huku baadhi ya vyombo vya habari nchini Kenya vikiripoti kwamba vyumba vya wagonjwa mahututi nchini Kenya vinakaribia kujaa wagonja wa corona.

Utafiti wabaini Wakenya milioni 2.6 waliugua Covid

Idadi hiyo mpya inajiri huku utafiti uliofanywa ukibaini kwamba Wakenya milioni 2.6 tayari wana virusi vya corona, wanasayansi wameeleza baada ya kupima damu iliyotolewa kwa ajili ya protini inayotumika kwenye mfumo wa kinga.

Protini hiyo (antibody) hutengenezwa na mwili kwa ajili ya kushambulia virusi na bakteria, na uwepo wake kwenye damu unaashiria kuwa mtu huyo aliwahi kuwa na maambukizi- hata iwapo hakuwahi kuonesha dalili.
Utafiti wabaini Wakenya milioni 2.6 waliugua Covid
Watafiti kutoka Taasisi ya utafiti wa tiba nchini Kenya wameunga mkono mfuko wa kuchangia damu uliofanyika nchi nzima kati ya mwezi Aprili tarehe 30 na tarehe 16 Juni.

''Kupimwa kwa antibodies kumeonesha kuwa Wakenya wengi tayari wamepata maambukizi kuliko ilivyokuwa ikibainika katika shughuli za upimaji nchini humo.,'' Ilieleza taasisi ya Kemri mapema wiki hii ikinukuliwa nan a gazeti la the Star nchini Kenya.

Kemri inakadiria kuwa karibu watu 550,000 jijini Nairobi na karibu 100,000 mjini Mombasa, tayari wameugua virusi hivyo na kupona na pengine kupata kinga.

Imeelezwa kuwa baadhi inawezekana waliathirika mapema mwezi Machi kwa kuwa protini hizo zinazopambana na virusi zinaweza kuwa kwenye damu kwa miezi kadhaa.

Idadi hiyo inaonesha kuwa Wakenya wameshuhudia idadi kubwa ya watu waliopata maambukizi halikadhalika vifo, taasisi hiyo ya utafiti ikikisia kuwa takriban watu 6,000 watakuwa wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa wa Covid-19 nchi nzima, kutokana na idadi ya sasa ya vifo nchini humo kwa ujumla.

Kwa mujibu wa gazeti la The Standard media, sehemu ya ripoti ya taasisi ya Kemri ilisomeka kuwa katika mji kama Nairobi kwa mfano, idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa wakati utafiti ulipokuwa ukifanyika ni 2,732 ikilinganishwa na idadi ya 550,000 wanaokisiwa kuwa na maambukizi na mjini Mombasa watu 1,368 lakini watu 100,000 wanakisiwa kuwa na maambukizi kutokana na utafiti huo.

Comments