Bernard Membe arudisha kadi ya uanachama CCM

ALICHOKISEMA BERNARD MEMBE BAADA YA KUFUTWA UANACHAMA WA CCM ...
Aliyekuwa waziri wa mambo ya nje ya nchi wa Tanzania, na kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bernard Membe,amerejesha kadi ya uanachama wa Chama hicho.

Membe aliyesindikizwa na mkewe,ameandika pia barua kukishukuru chama hicho kwa wema wote waliomtendea.

Kiongozi huyo wa zamani amerudisha kadi ya uanachama ingawa Chama cha Mapinduzi kilishamfukuza uanachama .

Membe alidai kuwa taratibu za kichama hazikufuatwa, na hivyo bado alikuwa mwanachama halali wa CCM.

Hii leo Membe hajasema anaelekea chama gani cha siasa japo wiki iliyopita aliiambia BBC kuwa endapo upinzani nchini humo utaungana na kumwomba ajiunge atafanya hivyo.

Membe pia anatarajiwa kugombea urais mwezi Oktoba.

Wiki iliyopita, Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe alimualika Membe ajiunge na upinzani.

Tuhuma dhidi ya Membe ndani ya CCM

Membe alikuwa akikabiliwa na tuhuma za kukiuka maadili pamoja na viongozi wengine waandamizi wengine wawili makatibu wakuu wa zamani Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana, ambao wao hawajafukuzwa.

Makamba amesamehewa, huku Kinana akionywa kwa karipio.

Katibu Mwenezi wa CCM Humphrey Polepole alidai kuwa mwenendo wa Membe umekuwa si wa kuridhisha toka mwaka 2014.

"Kamati Kuu imeazimia kwa kauli moja kwamba Bernard Membe afukuzwe uanachama wa CCM. Uamuzi huu umekuja baada ya kuwa taarifa zake ndani ya chama zinaonesha mwenendo wake kutoka mwaka 2014 ambako katika chama amewahi kupata adhabu nyingine ambazo zingeweza kumsaidia kujirekebisha," alieleza Polepole.

Membe, Makamba na Kinana walipelekwa katika kamati ya maadili ya CCM mwezi Disemba mwaka jana, na taarifa ya chama hicho ilidai kuwa viongozi hao pamoja na makada wengine watatu ambao walisamehewa walikidhalilisha chama mbele ya Umma.

Makada ambao walitangazwa kusamehewa ni January Makamba, Nape Nnauye na William Ngeleja ambao wote walimuomba radhi mwenyekiti wa CCM na rais wa Tanzania John Pombe Magufuli.

Baadhi ya mazungumzo ya simu ya wanachama hao sita wa CCM yalivujishwa kwenye mitandao nchini Tanzania wakizungumzia masuala mbalimbali kukihusu chama na mwenyekiti wake.

Sehemu ya mazungumzo yaliyovuja ya Mzee Yusuf Makamba na Kinana ni pamoja na kuandaa taarifa ya malalamiko dhidi ya 'mawanaharakati' Cyprian Musiba ambaye wanamtuhumu kwa 'kuwadhalilisha' bila kuchukuliwa hatua yoyote na kuhoji analindwa na nani?

Unaweza kutazama
Picha:Bernard Membe.jpg - Wikipedia, kamusi elezo huru
Madai ya hujuma

Kwa upande wa Membe, licha ya kusikika kwenye mazungumzo hayo yaliyovuja, amekuwa pia akituhumiwa na baadhi ya wanchama wa chama hicho kuwa najipanga 'kumhujumu' Magufuli katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

Membe amekuwa akihusishwa kwa muda mrefu na mipango ya kutaka kugombea tiketi ya urais kupitia CCM mwaka huu, hatua ambayo baadhi wanaitafsiri kama usaliti.

Japo katiba ya CCM inaruhusu hilo, imekuwa ni ada ya chama kumuachia rais aliye madarakani kupita bila kupingwa kwa awamu ya pili ya urais.

Wakati huo tukio hilo lilitafsiriwa kwamba kufukuzwa kwa Membe ni kutokana na kuhusishwa huko na mipango ya Urais.

Comments