Manara afunguka ‘TP Mazembe ndege sio yao wamekodisha, tunampiga tatu, AS Vita wameanza kufungwa kabla kuingia uwanjani’

Msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara amesema kuwa maandalizi yao yapo vizuri kuelekea mchezo wao wa robo fainali ya klabu bingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe huku Emmanuel Okwi, Clatous Chama, Meddie Kagere, John Bocco, Erasto Nyoni na Shomari akisema wapo kwenye mazoezi na kuongeza Mazembe hawakuja na ndege yao binafsi.


Manara ameyasema hayo kupitia kipindi cha Wednesday Night Live kinachorushwa na Azam Tv .

”Maandalizi yetu yapo vizuri na tumepata muda kidogo kwa wachezaji kupumzika. Tunatarajia mchezo wa Jumamosi tutapata matokeo chanya ili kwenda Lubumbashi tukiwa na mtaji mzuri wa kutosha ambao utatuwezesha kufuzu kucheza nusu fainali ya klabu bingwa Afrika, TP Mazembe Dar es Salaam tatu (thalatha) hazi pungui kwa namna yoyote ile.” msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara.


Haji Manara ameongeza ”Wachezaji wetu wote wapo wako vizuri, Emmanuel Okwi, Clatous Chama, Meddie Kagere, John Bocco, Erasto Nyoni na Shomari wote wapo na wanaendelea na mazoezi hatuna shida.”

”Lengo letu lilikuwa ni kucheza hatua ya makundi, tumevuka tumeingia hatua ya robo fainali tunaona nafasi ya kufanya vizuri zaidi kwenye klabu bingwa Afrika zipo, kwa sababu hawa tunaocheza nao wanafungika. Simba ile iliyofungwa na Mazembe 2011 siyo hii na wao siyo hawa waliyokuwa leo.”

”Mazembe wameingia wanatishiana tishana ndege yao binafsi, kwanza siyo kweli ndege ile wamekodisha, kwasababu wao lazima wawasiliane na sisi na sisi ndiyo tunawapokea kama sisi ambavyo tutawapa taarifa tutakavyokwenda, lakini hata wakija na ndege yao binafsi sisi inatusaidia nini ?.”

”Saoura walikuja na ndege kutoka kwao mpaka Dar es Salaam wamekula tatu hapa, kwanza ukija na ndege yako mwenye sisi ndiyo tunapenda tunakupiga tatu bora wangekuja na dala dala, Simba unatutisha na ndege sisi ndiyo timu ya kwanza Afrika Mashariki kupanda ndege mwaka 1939.”

”AS Vita wameanza kufungwa kabla hawajaingia uwanjani, na aliyowaponza anajulikana Zahera.”

Simba SC wanatarajiwa kuingia uwanjani siku ya Jumamosi kuwakabili TP Mazembe kwenye mchezo wa klabu bingwa barani Afrika hatua ya robo fainali.

Comments