Waziri Mkuu ampa siku 16 Murugenzi Rombo

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa siku 16 kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Magreth John awe amepeleka asilimia 20 sawa na milioni 114 ya Kijiji cha Holili kabla ya March 10, 2019, fedha hizo zinatokana na mauzo ya madini ya pozolana.


Ametoa maagizo wakati akizungumza na watumishi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Holili pamoja na wananchi wa kijiji cha Holili, akiwa katika ziara yake ya kikazi Mkoani Kilimanjaro. Kituo hicho kipo katika mpaka wa Tanzania na Kenya.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo baada ya wananchi wa kijiji cha Holili kuwasilisha malalamiko yao kupitia mabango wakimuomba awasaidie ili Halmashauri hiyo iweze kulipa fedha zao zinazotokana na mapato ya mauzo ya madini hayo yanayochimbwa kijijini kwao.

“Mkuu wa wilaya (Agness Hokororo) simamia kuhakikisha kiasi hicho cha fedha kinakwenda kwa wananchi na Mkuu wa Mkoa (Dkt. Anna Mgwira) nataka nipate taarifa kuwa fedha hizo zimeshalipwa kwa uongozi wa kijiji husika.” Waziri Mkuu

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watendaji katika maeneo mbalimbali nchini kuwa wamepelekwa huko kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, hivyo hawana budi kutenga muda wa siku tatu kwa wiki na kwenda maeneo ya vijijini kusikiliza kero zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.


Comments