Uchaguzi Nigeria 2019: Je wapiganaji wa Boko Haram wameshindwa?

Mji mmoja katika eneo la kaskazini mwa Nigeria
Boko Haram wameimarisha mashambulizi yao wakati huu ambapo Nigeria inajiandaa kwa uchaguzi mkuu

Wanamgambo wa kundi la Boko Haram wamekuwa wakiwahangaisha watu katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria kwa zaidi ya mwongo mmoja.

Rais Buhari anasema shughuli za kundi hilo zimedhibitiwa tangu alipoingia madarakani mwaka 2015.

Wapinzani wake wa kisiasa wanapinga kauli hiyo wakisema hali imezidi kuwa mbaya ikizingatiwa idadi ya mashambulizi na visa vya utekaji nyara vinavyofanywa na kundi hilo.

Taifa hilo linapojiandaa kwa uchaguzi mkuu utakaofanyika Februari 16, Kitengo cha BBC Reality Check kimechanganua ukweli wa mambo kuhusu hali ya usalama nchini Nigeria.

Kundi la Boko Haram lilibuniwa mwaka 2002 kwa lengo la kupigania maslahi ya waumini wa dini ya kiislam kaskazini mwa Nigeria, lakini kadiri muda ulivyosonga kundi hilo liligeuza na kuanza kutumia mbinu za itikadi kali kufikia malengo yake.

Rais wa Nigeria Muhammadou Buhari
Rais wa Nigeria Muhammadou Buhari
Kando na Nigeria kundi hilo pia linaendesha shughuli zake katika mataifa jirani ya Chad, Niger na Cameroon.

Maelfu ya watu wameuawa na wengine wengi kufurushwa makwao katika muda wa mwongo mmoja uliyopita.

Mwaka 2014 wanamgambo wa Boko haram waliwateka nyara zaidi ya wasichana 200 wa shule ya Chibok, Kaskazini mashariki ya Nigeria na mpaka sasa hawajapatikana.

Mwaka 2015, kundi la Boko Haram liliorodheshwa kuwa kundi hatari zaidi la kigaidi duniani na Taasisi ya masuala ya uchumi na amani duniani.

Tangu wakati huo maeneo yanayoshikiliwa na kundi hilo yamepungua huku likidai kumeguka baada ya mgogoro wa uongozi kuibuka.

Hata hivyo wanamgambo wake wamekuwa wakiwahangaisha maafisa wa usalama ambao wanajaribu kuwatokomeza kwa kukabiliana nao kwa kila njia.

map

Hatua yao ya kuwateka nyara zaidi ya wasichana 100 katika mji wa Dapchi mwaka 2018 ilizua gumzo kali ikiwa kweli kundi hilo limeshindwa japo wasichana hao waliokolewa baadae.

Kauli zinazokinzana
Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, ambaye anamunga mkono mgombea wa upinzani, Atiku Abubakar, amemkosoa vikali rais Muhammadu Buhari kuhusiana na jinsi utawala wake ulivyoshugulikia suala la Boko Haram.

Zifahamu changamoto kuu za Nigeria katika ramani 9
"Usalama umezorota, watu wanatekwa kila mahali," alisema bwana Obasanjo mwezi Januari.

Lakini rais Buhari anasema wapiganaji wa Boko Haram "wamesambaratishwa" katika ngome yao tangu ilipoingia madarakani mwaka 2015.

Ukweli ni upi kuhusiana na mashabulio ya kundi hilo dhidi ya raia?
Zaidi watu milioni mbili wametoroka makwao kwa hofu ya kushambuliwa na Boko Haram, kwa mujibu wa UNHCR
Zaidi watu milioni mbili wametoroka makwao kwa hofu ya kushambuliwa na Boko Haram, kwa mujibu wa UNHCR
Mashambulio ya Boko Haram yamepungua?

Ukosefu wa usalama na miundo mbinu ya mawasiliano hasa katika maeneo ya vijijini umeifanya serikali na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kushindwa kunakili hali halisi ya mambo huku visa vingine vikosa kuripotiwa.

Kuanzia mwaka 2015 zaidi ya vifo vya watu 5,000, vimehusishwa na mashambulizi ya wanamgambo wa Boko Haram japo vifo hivyo vimepungua hadi 1,000 kwa mwaka katika miaka mitatu iliyopita.

Hali hiyo ilitokana hatua ya serikali kuzindua oparesheni ya kijeshi thidi ya kundi hilo kwa ushirikiano na jamii ya kimataifa.

Maaeneo mengi yaliyokuwa chini ya himaya ya Boko Haram yalikombolewa katika oparesheni hiyo.
Boko Haram killings graph
Kwa hivyo rais Buhari yuko sahihi anaposema mauji yanayofanywa na wanamgambo w kundi hilo yamepungua tangu alipoingia madarakani mwaka 2015.

Lakini mashambulizi hayajakomeshwa kabisa kwa sababu visa kadhaa vimeripotiwa mwaka 2019.

Baada ya kushindwa nguvu na kufukuzwa kutoka kwenye ngome yao wamegeukia mbinu nyingine ya kuvamia mashule, vijiji na kuwateka nyara watu.

Comments