Mwili wa Kijana uliokaa mochwari siku 260 hatimaye wazikwa leo (+picha)


Mwili wa Frank Kapange mwenye miaka 22 leo February 26,2019 umechukuliwa na familia yake katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya baada ya kukaa mochwari miezi nane na siku 22.

Msemaji wa familia, Julius Kapange amesema wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya Mahakama kuamuru wazike ndani ya wiki moja la sivyo Jiji lingezika.

“Leo tumefanikiwa kuchukua mwili wa kijana wetu, tunaenda kuzika kijijini kwetu Syukula Rungwe sababu ya kufanya hivyo ni kwamba Mahakama ilitutaka tuzike kabla ya wiki moja.” Kapange

“Hivyo tukaona ni vyema tufanye hivyo kuliko kuendelea kumtesa mwanetu lakini mpaka tumefika hatua hii Mahakama haijatutendea haki katika kuamua kesi yetu,” Kapange.

Kapange amesema siku ya Jumapili ya Februari 24,2019 waliitwa na Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ambapo waliambiwa wachukue mwili wa kijana wao na gharama za kuhifadhia maiti hiyo kwa muda wote wamesamehewa.

“Sisi tulienda mahakamani kuomba mwili wa mtoto wetu uchunguzwe kwani kifo chake kilikuwa ni cha utata na siyo kususia kama wengine wanavyosema na baada ya mazishi tutaendelea kufanya shughuli zingine za kimaendeleo,” Kapange.

Akizungumza kwa njia simu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Godlove Mbwanji amesema wameamua kusamehe gharama za kutunzia maiti hiyo kwa muda wote ili fedha ambazo waliziandaa zikatumike kwenye msiba.

Frank alifariki June 4, 2018 huku kifo chake kikigubikwa na utata kutokana na mazingira yake baada ya ndugu kudai kijana wao ambaye alikuwa ni mfanyabiashara wa nguo za mitumba soko la Sido jijini Mbeya kufariki kwa kipigo akiwa mikononi mwa polisi hivyo ndugu waligoma kumchukua na kwenda kumzika.




Comments