Waliomlawiti Mwanachuo na kumdai pesa wafikishwa mahakamani


Mfanyabiashara Samsoni Kisuguta (28) na Mwanafunzi wa Chuo cha Ardhi, Anna Mwaisumo (23) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka manne ikiwemo kumlawiti Mwanachuo (Jina Limehifadhiwa) na kushinikiza awape Pesa.

Washtakiwa hao ambao wanadaiwa kuwa wapenzi wamesomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono mbele ya Hakimu Mkazi, Ally Salum ambapo wanadaiwa kosa lao la kwanza ni kula njama ya kutenda katika tarehe tofauti na eneo mwaka 2017 ili kutenda kosa la kulawiti na kujipatia fedha.

Wakili Kombakono amedai kuwa kosa jingine ni kulawiti ambapo wanadaiwa wamelitenda December 10,2017 katika Guest ya Morgan jijini Dar es Salaam ambapo walimlawiti Mwanachuo (Jina Limehifadhiwa).

Kosa jingine ni kusambaza picha za Ngono, ambapo washtakiwa hao wanadaiwa October 7,2018 maeneo ya jijini la Dar es Salaam walichapisha kupitia makundi ya Whatsapp picha za ngono za Mwanachuo huyo (Jina Limehifadhiwa) huku wakijua ni kinyume na sheria.

Pia washtakiwa hao wanakabiliwa na kosa la kudai Pesa ili wasisambaze picha za ngono, ambapo wanadaiwa walilitenda November 13, 2018 wakiwa jijini Dar es Salaam ambapo walijipatia fedha taslimu Sh.250,000 kutoka kwa Mwanachuo huyo ili wasisambaze picha zake za Ngono walizompiga.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, wakili Kombakono amedai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika ambapo washtakiwa hao walikana makosa hayo. Mahakama iliwapatia washtakiwa masharti ya dhamana  ya kuwa na wadhamini wawili wataosaini Bondi ya Laki Tano, lakini hawakuyatimiza.Kesi imeahirishwa hadi January 3,  2019.

Comments