Serikali ya Marekani kutetea marufuku Mahakama ya Juu

Waandamanaji Seattle, Washington on May 15, 2017
Marufuku hiyo ilisababisha maandamano maeneo mbalimbali Marekani
Ikulu ya White House imeiomba Mahakama ya Juu nchini Marekani kurejesha tena marufuku ya usafiri iliyokuwa imewekewa watu kutoka mataifa kadha yenye Waislamu wengi na serikali ya Donald Trump.
Marufuku hiyo ilisitishwa na mahakama za ngazi za chini ambazo zilisema ina ubaguzi.
Maombi mawili ya dharura sasa yamewasilishwa na serikali ya Bw Trump kwa mahakama hiyo yenye majaji tisa, kuwaomba wabatilishe uamuzi wa mahakama hizo za ngazi ya chini.
Kutangazwa kwa marufuku hiyo kulizua maandamano maeneo mbalimbali Marekani pamoja na kuzua mjadala mkali.
"Tumeiomba Mahakama ya Juu kusikiliza kesi hii muhimu na tuna imani kwamba amri hii kuu, alipokuwa akiitoa Rais Trump, alitumia mamlaka yake ya kikatiba aliyopewa kulilinda taifa hili na jamii za Wamarekani dhidi ya ugaidi," alisema msemaji wa Wizara ya Haki Sarah Isgur Flores.
"Rais hatakiwi kuwapokea watu kutoka nchi ambazo zinafadhili au kuwalinda magaidi, hadi athibitishe kwamba wanaweza kukaguliwa ipasavyo na kuhakikisha hawahatarishi usalama wa Marekani."

Amri kuu ya kwanza ya Bw Trump aliyoitoa Januari ilisitishwa baada ya kesi zilizowasilishwa na majimbo ya Washington na Minnesota.
Baadaye, alitoa amri nyingine aliyoifanyia mageuzi kidogo na kuzuia watu kutoka Somalia, Iran, Syria, Sudan, Libya na Yemen kupewa viza za kuingia Marekani.
Kadhalika, alizuia kwa muda wakimbizi wasiingie Marekani.
Hata hivyo, mahakama Maryland iliamua marufuku hiyo ilikiuka haki za kikatiba na kutoa agizo la kusitisha kwa muda utekelezaji wake.
Jaji mwingine Hawaii pia aliunga mkono wapinzani wa marufuku hiyo waliosema inabagua, na kusema Serikali haikutoa ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba marufuku hiyo ni hitaji la usalama wa taifa.
Mwezi uliopita, mahakama ya rufaa Virginia ilikataa kuondoa agizo la muda la kuzuia utekelezwaji wa marufuku hiyo.

Comments