Wanajeshi waasi wafyatua Risasi miji Mikuu Ivory Coast

Wanajeshi hao waasi Bouake, Mei15, 2017.
Wanajeshi hao waasi wamesema hawako tayari kwa mazungumzo
Wanajeshi wanaogoma nchini Ivory Coast wamefyatua risasi katika miji minne mikubwa nchini Ivory Coast na kupuuza amri ya serikali ya kuwataka waweke chini silaha zao.
Milio ya risasi ilisikika karibu na ikulu ya rais katika mji mkuu Abidjan, na katika mji wa pili kwa ukubwa wa Bouaké, pamoja na miji mingine muhimu kwa sekta ya kakao nchini humo.
Benki kote nchini Ivory Coast zimefungwa.
Wanajeshi hao waasi, waliosaidia Alassane Ouattara kuingia madarakani mwaka 2011, wamekuwa wakizozana na serikali kuhusu kulipwa malimbikizi ya marupurupu.
Waasi hao wa zamani ni karibu 8,400 na walijumuishwa katika jeshi la nchi hiyo ambalo sasa lina wanajeshi 22,000.
Mkuu wa majeshi ya nchi hiyo Jenerali Sékou Touré ameapa kumaliza maasi hayo, ambayo yalitokana na mzozo kuhusu malipo.
Kupitia taarifa Jumapili, Jenerali Touré alisema wengi wa wamnajeshi hao waliogoma walikuwa awali wameitikia wito wa kuwataka wasitishe mgomo wao.
 
Lakini operesheni ya kijeshi imeanzishwa kwa sababu baadhi ya wanajeshi wameendelea kupuuza maagizo ya wakuu wao, amesema.
Wanajeshi hao waasi wameapa kujibu mashambulio iwapo watakabiliwa na wanajeshi watiifu kwa serikali.

Wanajeshi waasi mjini Bouake, Mei 14, 2017
Wanajeshi hao waasi walimsaidia Ouattara kuchukua uongozi 2011
Milio ya risasi pia imesikika katika kambi ya jeshi ya Akouédo, mtaa ambao huwa na wakazi wengi wa mapato ya wastani nchini Ivory Coast na ambapo pia raia wa kigeni hupenda sana kuishi.
Mwanajeshi aliyegoma Bouake, Mei 14, 2017
Wanajeshi waliogoma wanadhibiti mji wa Bouaké, mji wa pili kwa ukubwa Ivory Coast
Serikali imepungukiwa na pesa kutokana na kushuka kwa bei ya zao la kakao, jambo linaloifanya vigumu kwa serikali kutimiza madai ya wanajeshi hao.
Mzozo huo wa sasa umezua wasiwasi wa kuzuka tena kwa ghasia zilizoshuhudiwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka kumi nchini Ivory Coast, ambavyo vilimalizika mwaka 2011.
Wengi wa wanajeshi hao waasi, ambao walianza kuasi Januari, ni waasi wa zamani ambao walijiunga na jeshi baada ya kumalizika kwa vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe.
Walimsaidia Rais Alassane Ouattara kuchukua uongozi 2010 baada ya mtangulizi wake Laurent Gbagbo kukataa kushindwa katika uchaguzi mkuu.
map
Walianza kuasi mara ya kwanza Januari na kuilazimisha serikali kuahidi kuwalipa jumla ya $8,000 (£6,200) kila mmoja kama sehemu ya malimbikizi ya marupurupu.
Walitarajiwa kupokea malipo zaidi mwezi huu na baadhi ya wanajeshi walikasirika kwamba msemaji wao Alhamisi alisema watatupilia mbali madai yao ya kutaka kulipwa pesa zilizosalia.
 
Serikali imesema haitafanya mazungumzo na wanajeshi hao.
Ivory Coast ndiyo mzalishaji mkubwa zaidi wa kakao duniani, na zao hilo hutegemewa sana na taifa hilo kujipatia fedha za kigeni.

Ivory Coast mji wa Bouake, Mei 15, 2017.
Mji wa Bouaké umekuwa kitovu cha maasi
Waasi Bouake, on May 15, 2017.
Serikali inasema haina pesa za kuwalipa wanajeshi hao

Comments