BUNGE LA UINGEREZA LAUNGA UCHAGUZI MKONO UCHAGUZI WA MAPEMA

Wabunge wameunga mkono hoja ya Waziri Mkuu Theresa May

Ni rasmi sasa uchaguzi Mkuu wa Uingereza utafanyika Juni nane mwaka huu. Hii ni baada ya wabunge kuunga mkono hoja ya Waziri Mkuu Theresa May kufanya uchaguzi wa mapema.
Bunge la Uingereza limeunga mkono kwa kura 522 dhidi ya 13. Vyama vya upinzani vimeunga mkono hoja ya Waziri Mkuu.
Bi Theresa May, ametaka idhini kutoka kwa raia wa Uingereza katika kuendeleza mazungumzo ya mchakato wa Uingereza kuondoka Muungano wa Ulaya.
Kiongozi wa upinzani Jeremy Corbyn ameunga mkono uchaguzi wa mapema huku akimlaumu Waziri Mkuu kwa kutotekeleza ahadi zake kwa raia.

Uchaguzi Mkuu wa Uingereza ulipangwa kufanyika mwaka wa 2020. Hata hivyo bunge linaweza kufanyia sheria ya uchaguzi marekebisho kutoa nafasi ya uchaguzi wa mapema.

Waziri Mkuu anatarajiwa kuanza kunadi chama chake cha Conservatives. Aidha vyama vingine vimeanza kampeini kuhakikisha vinaongeza wingi wa wabunge.

Chama kitakachopata wabunge wengi kitaunda serikali na Waziri Mkuu atakua na wajibu kuamua mkondo ambao Uingereza itafuata katika kujiondoa Muungano wa Ulaya.
Bunge litavunjwa hapo mwezi Mei.

Comments