MISS TANZANIA MAJANGA..LUNDENGA AKWAMA MAHAKAMANI


NA FLORA MWAKALASA - HABARI LEO.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imetupilia mbali pingamizi la awali lililowasilishwa na mwanzilishi wa mashindano ya urembo ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga dhidi ya ombi la kuzuiwa kuendelea kuendesha mashindano hayo yanayotarajiwa kufikia kilele chake Oktoba 11, mwaka huu.
Hakimu Mkazi Frank Moshi alitoa uamuzi huo jana baada ya kupitia hoja za pingamizi hilo lililowasilishwa na Lundenga kupitia kwa Wakili wake Audax Kahendaguza.
Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Moshi alitupilia mbali pingamizi la kusikilizwa kwa ombi lililowasilishwa na mwanzilishi mwenzake wa mashindano hayo, Prashant Patel na kuamuru lianze kusikilizwa.

Katika pingamizi lake, Lundenga alidai mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa amri iliyoombwa Patel kwa kuwa alichoomba siyo zuio la muda, bali la kudumu, pia vifungu vya sheria alivyotumia siyo sahihi kuiwezesha Mahakama kusikiliza.

Aidha, alidai ombi hilo limeletwa kabla ya muda wake kwa sababu kwa mujibu wa mkataba, Lundenga alitakiwa kumlipa Patel siku tano kabla ya mashindano, lakini yameletwa siku nane kabla ya mashindano hayo, pia hati ya kiapo inayounga mkono ombi ina mapungufu kwa kuwa inajumuisha maoni na majumuisho ambayo hayatakiwi kisheria.

Patel aliwasilisha ombi chini hati ya dharura, kupitia kwa wakili wake Benjamin Mwakagamba, akidai Lundenga ana mpango wa kuendesha mashindano hayo kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, kinyume cha sheria na bila hata kumtaarifu.

Anaomba Mahakama itoe zuio la muda dhidi ya Lundenga, kuendesha mashindano hayo hadi shauri lake la msingi aliloliwasilisha litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi. Katika kesi ya msingi, Patel anadai pamoja na mambo mengine, utekelezaji wa makubaliano ya Februari 20, 2012 na malipo ya Sh milioni 19 ambayo hayajalipwa kwa mujibu wa mkataba na faida nyinginezo ambazo zimejitokeza hadi Septemba 23, mwaka huu.

Katika hati ya kiapo inayounga mkono ombi hilo, Patel anadai kuwa yeye pamoja na Lundenga ndiyo waanzilishi, waongozaji na waendeshaji wa mashindano ya Miss Tanzania na wamekuwa katika hali hiyo kwa miaka 20 sasa, tangu mashindano hayo yaliporuhusiwa tena mwaka 1994. Kwa kipindi chote hicho, wamekuwa wakisaini makubaliano ya namna ya kuendesha mashindano hayo na mara ya mwisho walisaini makubaliano Februari 20, 2012, lakini Lundenga alikataa kusaini makubaliano kwa mwaka 2013 na 2014 na ameshindwa kumlipa fedha zake Sh milioni 19 badala yake ameshirikiana na wadhamini wengine kuendesha mashindano hayo.

Kwa mujibu wa makubaliano, Lundenga pia alipaswa kulipa pauni za Uingereza 30,000 kama malipo ya kibali kwa mwendeshaji wa shindano hilo duniani, Miss World, deni ambalo limekuwa la muda mrefu, hivyo kuchafua hadhi. Baada ya uamuzi wake, Hakimu Moshi, kesi hiyo ilianza kusikilizwa jana mchana na itaendelea leo.
CHANZO HABARI LEO

Comments