SABABU 10 ZILIZOMTOA KOCHA LOGARUSIC

 
Kocha, Zdravko Logarusic akiwapa maelekezo wachezaji wa Simba kabla ya kutimuliwa
SIMBA ilimpa kocha, Zdravko Logarusic, mkataba wa mwaka mmoja wiki tatu zilizopita. Lakini juzi Jumapili ilifanya uamuzi mgumu kwa kumpiga chini kwa maelezo kwamba haendani na hali halisi ya klabu.

Kabla ya kumtimua Logarusic, uongozi wa klabu hiyo ulipiga hesabu kali. Kocha huyo alichukua Dola 24,000 (Sh 39.7milioni) ambazo ni ada ya kusaini mkataba na ili kuuvunja mkataba anatakiwa alipwe Dola 5,000 (Sh8.1 milioni).

Viongozi hao wakaona ni bora kupoteza Sh 47.8 milioni kuliko kuangamiza kiasi cha Sh3 bilioni na kuambulia patupu kwenye Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Simba imepanga kutumia bilioni hizo msimu ujao, ni fedha nyingi, zinawauma viongozi wa klabu hiyo na ni dhahiri kuwa wanataka timu yao ifanye vizuri baada ya kutumia fedha hizo na si kitu kingine. Tathmini hiyo ya hesabu ilionyesha kuwa kocha Logarusic haendani na kasi yao, makosa yake yamekuwa ni yale yale siku zote na amekuwa habadiliki. Wachezaji wanaonekana kumchoka hivyo kuokoa jahazi, wakafanya maamuzi magumu.

Mwanaspoti ambayo ilikuwa ikifuatilia nyendo za kocha huyo kwa karibu tangu ajiunge na klabu hiyo inakuletea sababu 10 zilizomwonyesha mlango wa kutokea;

Ukali uliopitiliza

Ukiwa katika uongozi sehemu yoyote unahitaji kuwa mkali kwa baadhi ya mambo, lakini usisahau kutumia busara.

Logarusic alikuwa mkali, busara kwake ni kitu cha mwisho, mchezaji akikosea kidogo alikua akijuta. Ukali wake ulipitiliza hadi baadhi ya wachezaji waliogopa. Hali hiyo iliwachosha viongozi waliokuwa wakimwomba apunguze, japo hakuwasikiliza.

Kulazimisha mambo

Kocha Logarusic anaiamini akili yake kwa asilimia 100, ana amini kila akifanyacho ni sahihi, ni mgumu kutekeleza maoni ya wengine. Imani hiyo ilimfanya awe na tabia ya kulazimisha mambo. Tabia hiyo ilimfanya Loga kuwatema wachezaji 12 kwenye kikosi chake, ni idadi kubwa ya wachezaji lakini alilazimisha hadi yakatimia, Uhuru Selemani pekee ndiye aliyesalimika tena kwa jitihada zake mwenyewe na za baadhi ya viongozi. Uongozi ukaona kuburuzwa.

Wachezaji wa Mbeya City

Kabla ya kwenda mapumzikoni kwao Croatia, Logarusic alipendekeza klabu hiyo isajili wachezaji kadhaa kutoka Mbeya City wakiwamo Deus Kaseke, Saady Kipanga na Anthony Matogolo. Aliporejea hakumkuta hata mmoja wao kikosini hapo, akaanzisha varangati akitaka wasajiliwe.

Kitendo hicho kiliwakera viongozi wa timu hiyo kutokana na ukweli kwamba kumsajili mchezaji mmoja kutoka Mbeya City ni gharama kubwa wakati klabu hiyo ingeweza kumpatia kocha huyo wachezaji wenye vigezo anavyovitaka kwa kiasi kidogo tu cha fedha.

Wachezaji vijana wa Simba

Kocha Logarusic hawakubali wachezaji vijana wa klabu hiyo licha ya uwezo mkubwa walionao. Logarusic amekuwa hawakubali wachezaji kama Abdallah Seseme, Said Ndemla, Ibrahim Twaha na hata wakati mwingine Ramadhani Singano ‘Messi’. Kocha huyo pia amekuwa hawakubali wachezaji Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Hussein Sharrif ‘Casillas’ waliosajiliwa kikosini hapo kwa madai kuwa bado ni wadogo kucheza Simba. Kitendo hicho kiliwakera viongozi wa klabu na baadhi yao waliapa kuwa kuliko kocha huyo aendelee kuwakebehi wachezaji hao ambao wametengenezwa Simba ni bora atimke zake na ndicho kilichotokea.

Ashindwa kuelewana na Matola

Habari za ndani kutoka Simba zinaeleza kuwa Logarusic alikuwa hasikilizi ushauri wowote kutoka kwa msaidizi wake Selemani Matola. Kitendo hicho kilimkera Matola ambaye aliamua kujitoa na kumwacha kocha huyo atekeleze kila analolitaka hata kama aliona sio sahihi, huo ulikuwa uamuzi wa busara kuepusha migogoro. Ingawa uongozi uliona ukaamua kuchuna.

Loga alifanya kosa kubwa hapa kwani hafahamu historia ya Matola kwenye kikosi cha Simba wakati akiwa mchezaji, hafahamu namna viongozi wa Simba wanavyomkubali nahodha huyo wa zamani wa kikosi chao.

Akili yote kwa Hans Poppe

Habari za ndani kutoka Simba zinaeleza kuwa baada tu ya Logarusic kutua nchini Desemba mwaka jana alifanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe ambaye ndiye aliyemshawishi kuifundisha klabu hiyo.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa baada ya Loga kufahamu utajiri na ushawishi aliokuwa nao Hans Poppe ndani ya Simba alikuwa akimheshimu kigogo huyo na kuwadharau wengine. Kitendo chake cha kuwabagua vigogo kiliwakera wengine.

Maadili mabovu nje ya uwanja

Kwa Ulaya ni jambo la kawaida kocha kujirusha kwa sana na kula bata anavyotaka.

Lakini Bongo ni shida kidogo. Loga ni mtu wa kujirusha na habari zinadai baadhi ya wachezaji walikuwa wakiviona vitendo vyake kwenye sehemu za starehe na kumshusha hadhi.

Mgogoro na Owino

Mapema mwaka huu aliingia katika mgogoro na nahodha wa sasa wa timu hiyo, Joseph Owino raia wa Uganda baada ya kocha huyo kumtolea mchezaji huyo lugha chafu mazoezini. Owino alikasirika na kumjibu kitendo kilichopelekea kocha huyo kumtimua kwenye mazoezi yake. Baadaye walisuluhishwa na mambo yalikwenda vizuri lakini tayari ilishakuwa dosari.

Aveva hawakubali makocha Wazungu

Inadaiwa kwamba Rais wa Simba, Evans Aveva, anaamini katika soka la Kiafrika, anaamini katika makocha Waafrika kwa hoja kuwa wanalitambua soka la Afrika vizuri na wanazifahamu hali halisi za timu za Kiafrika na hata gharama zao si kubwa.

Mapenzi hayo ya Aveva yamemfanya kutokuwakubali makocha wazungu kabisa na kama kocha Logarusic asingekuwa ameondoka na ‘kishika uchumba’ (Advance) baada ya kumalizika kwa msimu uliopita basi kocha huyo asingepewe mkataba wowote mpya klabuni hapo.

Katika kulithibitisha hilo Simba tayari imeanza mazungumzo na Mzambia Patrick Phiri ili kuziba pengo la Logarusic na endapo hilo litashindikana ndipo wanaweza kumrejesha Milovan Cirkovic aliyewahi pia kuinoa klabu hiyo.

Cirkovic anaweza kurejeshwa tu kwa hoja kwamba aliifundisha Simba kwa mafanikio lakini pia anaamini katika soka la vijana na ana uwezo mkubwa wa kuwatengeneza wachezaji kisaikolojia.

Sokomoko baada ya mechi ya Zesco

Hii ni sababu ya mwisho kabisa lakini imekuwa ya kwanza kumuondoa Simba. Huu ndiyo upenyo uliokuwa unatafutwa na watu waliokuwa tayari wana sababu zaidi ya tisa za kumtimua. Baada ya kumalizika kwa mechi ya Jumamosi dhidi ya Zesco ya Zambia Logarusic aligusa kidonda.

Alikaa na wachezaji ambapo aliwatukana, alimwambia Amri Kiemba na baadhi ya wachezaji wengine waende wakatafute timu za Ligi Daraja la Kwanza kama wameshindwa kuichezea Simba. Kila mchezaji alipewa yake.

Kipigo cha mabao 3-0 kutoka wa Zesco hakikuwa kitu kwa viongozi hao bali kikao hicho ndicho kilichohitimisha maisha ya Logarusic Simba.

Jumapili Asubuhi viongozi hao walikutana kwenye Hoteli ya Serena, Dar es Salaam na kupitia makosa ya kocha huyo na kuamua kwa kauli moja kuwa ni bora wamtimue.
Hapa ndipo palipobadilisha sifa ya Logarusic kutoka Kocha wa Simba hadi Kocha wa zamani wa Simba.





Comments