NILIGOMA KUMPA MZIMBA TIMU


FRED Mbuna ni miongoni mwa mabeki waliofanya kazi na Yanga miaka mingi. Amepitia mikononi mwa makocha mbalimbali akiwa kama nahodha kwa miaka 11 mfululizo hiyo ilitokana na nidhamu aliyokuwa nayo ndani ya kikosi hicho.

Mbuna alisajiliwa Yanga akitokea timu ya Majimaji ya Songea ambapo aliachana na Wanajangwani hao 2010 alipokwenda Moro United huku akiwa ni mchezaji aliyeondoka akiwa na heshima kubwa ndani ya klabu hiyo.

Mwanaspoti lilifanya mahojiano na Mbuna na alielezea mambo mbalimbali aliyowahi kukutana nayo akiwa na Yanga huku akilazimika kuyafanya japo mengine yalikuwa magumu.

Mbuna aliingia Yanga baada ya kuzichezea timu ya Nazareth, Lipuli na Majimaji ambayo baadaye alirudi tena kuisaidia katika Ligi Daraja la Kwanza msimu uliopita.

Kwa kipindi chote alichocheza Yanga hawakuwahi kutuhumiwa kuhujumu timu jambo ambalo amedai kuwa alitamani siku moja atuhumiwe kwa kuchukuwa fedha kwani wengi waliogopa kumpenyezea mlungula kutokana na heshima aliyokuwa amejiwekea.

“Mwaka 2010 baada ya kuondoka Yanga nilijiunga na timu ya Moro United wakati huo ipo chini ya Kocha Hassan Banyai, lakini nilicheza miezi mitano tu na kuondoka kwa sababu sikuendana na mfumo wao,” anaeleza.

Ushirikina

“Imani za kishirikina zipo kila sehemu na si kwa timu moja, ni kweli mengi yalifanywa wakati huo na nilitakiwa kwenda na mazingira yaliyopo,hivyo nikiambiwa nibebe kitu nikaweke sehemu fulani nilifanya hivyo hata kupelekwa kufanya mambo hayo nilienda.

“Nilikuwa nafanya kwa sababu wao wanaamini hivyo ila mimi sikuamini kama kweli kuna mafanikio kupitia mambo hayo ya kishirikina, sikuwa na imani nayo kabisa pamoja na kufanya na niliwekwa kipaumbele kwa sababu nilikuwa nahodha kila jambo lilikuwa ni lazima nishirikishwe.

“Ni hatari lakini sikuwa na sababu ya kuanza kubishana nao, nilifanya kwa kuwafurahisha wao waliokuwa wanaamini ili mradi sikuathirika na niliwashauri wenzangu wafanye ili kuwafurahisha viongozi na kuepuka kuonekana hawana nidhamu,” alisema.

“Viwango vinashuka sasa kwa sababu hakuna nidhamu, wengi wameweka starehe mbele kuliko soka, si kwamba enzi zetu hakukuwa na starehe ila tuliweza kutofautisha muda wa starehe na muda wa uwanjani hasa mazoezi.

“Nidhamu mbovu inachangia kushuka kwa viwango vya wachezaji kwa asilimia kubwa, wengi wanalalamika wanaonewa ama hawapangwi lakini utapangwa vipi wakati nidhamu yako mbovu, ni lazima wabadilike,” anasema.


Comments