MAXIMO ANOGEWA NA YANGA


KOCHA Mkuu wa Yanga, Mbrazili Marcio Maximo, ametamka kuwa amepata kombinesheni tano za washambuliaji hatari alizozipa jina la Yanga Best Five, lakini akasisitiza ametenga dakika 450 zitakazokiweka kikosi chake tayari kwa lolote.

Keshokutwa Jumatatu Maximo ataambatana na wachezaji 28 kwenda Pemba kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara na michuano kimataifa.

Ameliambia Mwanaspoti kuwa kombinesheni hizo ni kati ya Mbrazili Genilson Santos ‘Jaja’ na Jerry Tegete, Hussein Javu na Said Bahanuzi, Mganda Hamis Kiiza na Jaja, Kiiza na Javu pamoja na Kiiza na Tegete.

 Kombinesheni yoyote kati ya hizo inaweza kuanza kucheza kikosi cha kwanza kulingana na mfumo atakaoutumia katika mchezo husika ili kupata ushindi ndani ya dakika 90 za mchezo.

Amesema awali alitengeneza kombinesheni mbili kati ya Jaja na Tegete na Javu alipikwa na Bahanuzi.

“Ni kweli nilikuwa nimetengeneza kombinesheni ya Jaja na Tegete ambayo ilionekana kuwa nzuri, nimeendelea kutengeneza nyingine na mpaka sasa nimepata kama tano hivi zinazofanya vizuri,” alisema.

“Kombinesheni hizi nitazitumia kutokana na uzito wa mechi na mfumo nitakaotaka kuutumia, hiyo itanisaidia kuweza kupata ushindi. Kuna wakati nitakuwa nikicheza mpira wa kasi ambao utanilazimu kubadili mastraika tofauti na pale ninapohitaji kucheza mpira wa pasi zaidi.

“Sina kikosi cha kwanza mpaka sasa na sitarajii kutafuta wachezaji 11 wa kuanza kwenye kikosi cha kwanza, natafuta wachezaji 20 watakaoweza kucheza kwenye kikosi cha kwanza. Hiyo ndiyo timu ninayoitaka na mpaka sasa idadi hiyo inaonekana kukamilika.”

Maximo amepanga kucheza mechi tano za kirafiki kabla ya kuanza msimu wa ligi. Mechi hizo ni sawa na dakika 450 na Yanga itakaa kambini siku 10 visiwan i humo. Akizungumzia mchezaji atakayetemwa katika kikosi chake kutokana na kuzidisha wachezaji wa kigeni, Maximo alisema: “Natoa kipaumbele kwa mchezaji anayependa kucheza Yanga, mchezaji mwenye mapenzi na timu na mwenye nidhamu, kwa kifupi ni kuwa nazungumza kwa wachezaji nilionao na si wale walio makwao, hao sina mpango nao.”

Yanga ina wachezaji sita wa kigeni ikiwa ni kinyume na taratibu za usajili za Ligi Kuu Bara ambayo inaruhusu kusajili wachezaji watano tu.

 Wachezaji wa kigeni wa Yanga ni Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza wote raia wa Uganda. Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima raia wa Rwanda pamoja na Wabrazili Jaja na Andrey Coutinho.

Awali kulikuwa na taarifa za kuachwa kwa Kiiza lakini kutokana na Okwi kutokuripoti kwenye mazoezi ya timu hiyo mpaka sasa, mambo yanaweza kugeuka lakini Maximo aliomba apewe muda hadi siku moja kabla ya kufungwa kwa usajili.

Comments