LOGARUSIC AONDOKA KWA MKWARA SIMBA


ALIYEKUWA Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic ameondoka nchini usiku wa kuamkia jana Jumatano akiwa na siri kubwa moyoni huku akiwaambia Wanasimba ‘Mtanikumbuka’.

Logarusic ambaye alikuwa kimya tangu alipositishiwa mkataba wake wikiendi iliyopita, alifanya mahojiano na Mwanaspoti dakika chache kabla ya kupanda ndege kurejea kwao Croatia huku akiwa makini na kusisitiza atakumbukwa.

Akizungumza Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Logarusic alisema: “Sina tatizo lolote na nashukuru kwa kuachishwa kazi maana ukiwa kocha hivi ni vitu vya kawaida kutokea. Kuhusu sababu za kutimuliwa kwangu, naona ni siasa tu ndiyo iliyotumika hakuna jipya, kosa langu ni kutokubali kuwa mwanasiasa katika soka.

“I came as a man, I act as a coach and I leave as a gentleman (Nilikuja kama mtu, nikaishi kama kocha na naondoka mwanaume), wanachama na mashabiki wa Simba watanikumbuka siku si nyingi kwa mambo niliyokuwa nayaandaa kwao na hata niliyofanya.”

Logarusic alisema sababu nyingi zilizoelezwa kuhusu kutimuliwa kwake, ni za kuhalalisha yeye kuondoka kwani hakuwa tayari hata kidogo kuona siasa inaingilia kazi yake.

“Naiacha Simba ikiwa na kikosi cha ubingwa, ndiyo kikosi hiki kinaweza kutwaa ubingwa na kama ningebaki nacho hakika ningechukua ubingwa. Najua kocha mpya atakuja lakini muda si mrefu wanachama wataujua ukweli na hapo ndipo nitakapokumbukwa,” alisema Logarusic.

Kuhusu tabia ya ukali kwa wachezaji, Logarusic alisema: “Nilikuwepo tangu mwanzo wa mwaka chini ya uongozi mwingine, sasa leo hii ndiyo naonekana mkali? Inawezekana lakini nilikuwa natekeleza majukumu yangu.

“Mimi ni binadamu hata hizo tabia zangu nje ya uwanja, ni mambo yangu binafsi hivi tukiangaliana mmoja mmoja ni nani aliyetimia? Sisi ni binadamu tuhukumu ambayo hata sisi hatuwezi kufanya.”

Logarusic ambaye amewahi kuzifundisha Hearts of Hoek ya Ghana na Gor Mahia ya Kenya, alijiunga na Simba Desemba mwaka jana na kuingoza katika mechi 21, kati hizo ameshinda nane, amefungwa nane na kutoka sare tano.

Comments