KOCHA PHIRI:YANGA LAZIMA WAKAE


KOCHA mpya wa Simba,Patrick Phiri, ameshtuka kusikia kuwa Mbrazili Marcio Maximo aliyekuwa akiinoa Taifa Stars yupo Yanga kwa sasa na atalazimika kukumbana naye timu hizo zitakapokutana kwenye mashindano mbalimbali yatakayozikutanisha msimu ujao.

Phiri akizungumza na Mwanaspoti hotelini alipofikia jijini Dar es Salaam jana Alhamisi, alionekana kushtuka alipoulizwa juu ya Maximo na akasema: “Kwani bado yupo Tanzania? ni kocha wa Yanga kumbe?”

Aliongeza kuwa Maximo ni rafiki yake na wanaheshimiana sana, lakini kwa sasa Mbrazili hiyo hana jinsi itabidi aishuhudie timu yake ya Yanga ikimaliza nyuma ya Simba.

Wakati Phiri akiwa kocha wa Simba msimu wa 2009/10 timu hiyo ilipomaliza msimu bila kufungwa, Maximo alikuwa akiifundisha Taifa Stars hivyo walikuwa wakifanya kazi kwa karibu ili kuisaidia timu hiyo ya Taifa, lakini sasa mambo yamegeuka kwani makocha hao watakuwa wakifundisha timu mahasimu.

“Yanga ni timu nzuri, inacheza mpira mzuri lakini itabidi wakubaliane na uhalisia kuwa Simba inarudi kwenye hadhi yake na Yanga italazimika kumaliza nyuma yetu, hiyo ndiyo njia pekee,” alisema Mzambia huyo.

“Binafsi nadhani wafurahie sisi kuwa mbele yao kwa sababu wakizubaa wanaweza kuwa tena nyuma ya timu nyingine, mechi tutakayokutana itabidi nihakikishe nawafunga, hapo ndipo mashabiki wa Simba wanapasubiri.”

Kocha huyo ana heshima kubwa Msimbazi baada ya kuipatia ubingwa mara mbili na kuisaidia timu hiyo kumaliza msimu bila kufungwa ambapo baada ya kuondoka kwake klabu hiyo ilifanikiwa kufanya vizuri kwa msimu mmoja pekee kabla ya kuporomoka na kumaliza kwenye nafasi ya nne msimu uliopita.

Aitamka Man United

Wapenzi wa Simba wanaweza wasimwelewe Phiri kwa hili kutokana na klabu ya Manchester United kumaliza katika nafasi ya saba msimu uliopita, lakini kocha huyo amesema anataka kuitengeneza klabu hiyo iwe kama Manchester United iliyochukua ubingwa mwaka juzi.

“Hapa ni kama mnanikumbusha Manchester United, ni timu yenye heshima, kikosi chake kimetengenezwa kwa muungano ambao unaisaidia timu kufanya vizuri kwa nyakati zote, hivyo ndivyo ninavyotaka Simba iwe,” alisema.

“Kwa muunganiko huu, timu itaweza kufanya vizuri kila mechi, itaweza kutoka nyuma na kuongoza katika mechi, si rahisi kuona timu inapoteza mchezo wakati  imeunganishwa kuanzia nyuma hadi mbele,” alisema Phiri.

Mkataba

Uongozi wa klabu hiyo umeamua kumpa Phiri mkataba wa mwaka mmoja ili aweze kutengeneza kikosi cha klabu hiyo kitakachoweza kuitoa jasho miamba mingine ya soka nchini na hata nje ya nchi.

“Nimesaini mkataba wa mwaka mmoja Simba, naelewa kuwa watu wana matarajio makubwa sana kwangu lakini watulie kwani mimi naifahamu Simba vizuri na nyakati zote nilizokuwa hapa walipata raha, watarajie raha zaidi kwa sasa,” alisema Phiri.

Rais wa Simba, Evans Aveva aliliambia Mwanaspoti mara baada ya kumalizana na Phiri, kuwa wamekubaliana na kocha huyo kuwa afanye kazi kubwa ya kuitengeneza timu yenye ushindani na ndipo malengo mengine kama ya kuchukua ubingwa yafuate.

“Tumempa kocha mkataba wa mwaka mmoja, lengo kubwa kwetu ni kutengeneza timu ya ushindani,tungeweza kumwambia kuwa atwae ubingwa kwa msimu ujao lakini tumefanya tathmini na kuona kuwa kikosi cha timu yetu kinahitaji kutengenezwa kwanza ili kiwe cha ushindani.

“Tunaimani kuwa hiyo kazi yeye anaiweza vizuri na ndiyo maana tumeamua kuwa naye,” alisema Aveva huku akitania kuwa Phiri atakaa Simba milele kwa kuwa wanamwamini na wanaiamini kazi yake.

Comments