AIRTEL RISING STAR INAKUJA

 
MASHINDANO mengine muhimu ya soka na yenye manufaa kwa soka la Tanzania yanaendelea nchini.


Mashindano haya yanashirikisha vijana wa umri chini ya miaka 17, ni mojawapo ya mashindano ya vijana wadogo ukiacha yale ya Copa Coca Cola ambayo hushirikisha vijana wa umri chini ya miaka 15 na Kombe la Uhai kwa vijana wa chini ya miaka 20.

Yote haya ni mashindano muhimu kwa maana ya kwamba yana mchango mkubwa katika maendeleo ya mpira wa miguu nchini Tanzania.

Ni mashindano ambayo yana maana kubwa katika suala zima la kuibua vipaji vya vijana wenye umri mdogo ambao kesho na keshokutwa wataweza kuwa tegemeo kwa Taifa Stars.

Mbali na mashindano hayo matatu, mashindano mengine ya vijana wa umri mdogo ni yale yanayoshirikisha shule za msingi na zile za sekondari ambayo yalifanyika hivi karibuni, Kibaha mkoa wa Pwani.

Pia kwa kuwa sasa tupo katika Airtel Rising Stars tunadhani huu ni wakati muafaka wa kukumbushana jambo la msingi ambalo linahitaji kuzingatiwa na kila aliyepewa dhamana ya kusimamia mashindano haya.

Jambo lenyewe ni kilio chetu cha mara kwa mara cha kutoona vijana wenye umri mkubwa au vijeba wanapata nafasi ya kushiriki mashindano ya vijana wa umri mdogo.

Ushiriki wa vijana wa aina hii unayafanya mashindano haya kutokuwa na maana na badala yake ule mtazamo wa kusaka vipaji unakosa mantiki.

Tunachotaka kukielezea hapa ni kwamba unapomshindanisha kijana mwenye umri chini ya miaka 17 na mwenye umri wa miaka 23, unawashindanisha watu wawili tofauti na hapo atakayeshindwa ni yule mwenye umri chini ya miaka 17.

Kwa hali hiyo kutumia vijeba kunaziba nafasi za vijana wanaofaa, vipaji vyao vinaachwa badala yake wanachukuliwa vijana ambao umri umesonga.

Hili ni tatizo kubwa na ambalo ni vyema juhudi zikafanyika likamalizwa kwa manufaa ya soka la Tanzania.

Kumshindanisha katika soka kijana mdogo mwenye umri chini ya miaka 17 na kijana mwenye umri wa miaka 23 au 24 kwetu tunakiona kitendo hiki ni kama dhuluma ambayo inatakiwa kukomeshwa kwa nguvu zote.

Comments